Muhtasari
Mwalimu alipogundua kwamba nina ujauzito, aliniita ofisini kwake na kuniambia, “Inabidi uondoke hapa shule mara moja kwa sababu una ujauzito.”
—Jamida K., Kahama, Tanzania, Aprili 2014.
Haturuhusu wasichana wajawazito kuendelea na shule. Tunamuelekeza arudi nyumbani na kisha kurudi shule baada ya kujifungua. Kama atakuja shule akiwa mjamzito atafanyiwa kejeli na wanafunzi wengine na kuwa mfano mbaya.
—Kenneth Tengani Malemia, naibu mwalimu mkuu, Shule ya Msingi Dyeratu, wilaya ya Chikwawa, Malawi, Septemba 2013
Bara la Afrika lina viwango vya juu vya ujauzito kwa vijana duniani, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Kila mwaka, maelfu ya wasichana wanapata ujauzito wakati ambapo walipaswa kuwa wanajifunza historia, aljebra na stadi za maisha. Wasichana wanaopata ujauzito wa mapema au bila kukusudia wanakutana na vikwazo vingi vya kijamii na kifedha vya kuendelea na elimu rasmi.
Wasichana wote wana haki ya kupata elimu bila kujali hali zao kama vile kuwa wajawazito, kuolewa au kuwa mama. Haki ya wasichana wajawazito na wakati mwingine wasichana walioolewa kuendelea na elimu imeibua majadiliano yenye hisia kali kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika miaka ya hivi karibuni. Mara nyingi mijadala hii imeegemea kujenga hoja juu ya “maadili,” kwamba mimba nje ya ndoa ni kinyume cha maadili, inayotokana na mawazo binafsi na uzoefu, na imani iliyojengeka kwa wengi kutokana na mafunzo ya dini juu ya ngono nje ya ndoa.Athari ya mijadala hii ni kwamba wasichana wajawazito na kiwango kidogo wavulana walioko shuleni na waliowapa mimba wasichana wanakumbana na kila aina ya adhabu, ikiwa ni pamoja na tabia ya ubaguzi ambayo inawanyima wasichana kufurahia haki yao ya elimu.Katika baadhi ya nchi zilizofanyiwa utafiti na ripoti hii, elimu inachukuliwa kama upendeleo ambao unaweza kuondolewa wakati wowote kama adhabu.
Hata hivyo matakwa ya kisheria kimataifa kwa serikali zote kutoa elimu kwa watoto wote bila ubaguzi yako wazi.
Mwaka 2013, nchi 55 ambazo zinaunda Umoja wa Afrika (AU) zilipitisha Ajenda 2063, mkakati wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa bara zima. Katika mkakati huu, serikali za Afrika ziliweka dhamira ya kujenga “mtaji wa rasilimali watu” wa Afrika, ambao uliutambua kama “rasilimali yenye thamani zaidi,” kupitia uwekezaji endelevu katika elimu, ikiwa ni pamoja na “kuondokana na tofauti za jinsia katika ngazi zote za elimu.” Miaka miwili baada ya kupitisha Ajenda 2063, serikali za Afrika ziliungana na nchi nyingine katika kupitisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), ajenda ya maendeleo ambayo inalenga kuhakikisha kwamba “hakuna anaebaki nyuma,” ikiwa ni pamoja na ahadi ya kuhakikisha elimu jumuishi na bora kwa wote. Serikali za Afrika vile vile zimepitisha malengo makubwa ya kumaliza ndoa za utotoni, kutambulisha elimu pana ya jinsia na afya ya uzazi, na kushughulikia kiwango kikubwa cha ujauzito wa utotoni barani kote ambao unaathiri vibaya elimu kwa mtoto wa kike.
Hata hivyo nchi wanachama wa AU watashindwa kufikia ahadi hii kama wataendelea kuwatenga maelfu ya wasichana kupata elimu kwa sababu ya kuwa wajawazito au kuolewa. Ijapokuwa nchi zote wanachama wa AU zimeweka dhamira ya kulinda haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kulinda haki ya kupata elimu kwa wasichana wajawazito na kina mama vijana, kiuhalisia kina mama vijana wanahudumiwa tofauti kulingana na nchi wanazoishi.
Idadi kubwa ya serikali wanachama wa AU wamepitisha sheria na sera ambazo zinalinda haki za mtoto wa kike kuendelea na masomo wakati wa ujauzito na hata wakati wa kulea ambapo anakuwa mama. Kuna sera na taratibu nzuri za kuangazia, na kwa kweli, nchi nyingi zinalinda haki za kina mama vijana kupata elimu katika sheria za nchi au sera kuliko kuwabagua. Nchi hizi zinaweza kuhamasisha nchi ambazo zinakosa sera za kutosha na kuwashawishi nchi chache ambazo zimepitisha au kuhamasisha hatua za adhabu na za kibaguzi dhidi ya kina mama vijana kupitisha sera zinazolinda na kuheshimu haki za binadamu.
Ripoti hii inatoa taarifa juu ya hali ilivyo katika sheria, sera na taratibu au mazoea ambayo yanazuia au kuwezesha wasichana wajawazito au walioolewa kupata elimu. Pia inatoa mapendekezo ya marekebisho yanayohitajika
Gabon, Kenya na Malawi ni miongoni mwa makundi ya nchi 26 za Afrika ambazo zimepitisha sera za “kuendelea” au “kujiunga upya” ili kuhakikisha kwamba wasichana wajawazito wanaweza kurudi kuendelea na shule baada ya kujifungua. Hata hivyo, utekelezaji na usimamizi hutofautiana katika nchi hizi, hususani kuhusiana na muda ambao msichana anaruhusiwa kutokuwepo shuleni, mchakato wa kujitoa na kujiunga, na uwepo wa miundombinu wezeshi mashuleni na katika jamii kwa mama kijana kubaki shule.
Ingawa mwenendo wa serikali nyingi zaidi kuamua kuwabakiza kina mama vijana shuleni ni imara, utekelezaji wa sheria na sera mara nyingi umekuwa hafifu, na usimamizi wa kina mama vijana kurudi kwenye elimu rasmi umeendelea kuwa dhaifu kwa ujumla. Vile vile kuna wasiwasi juu ya uwepo wa adhabu na vipengele vyenye madhara katika baadhi ya sera. Kwa mfano, baadhi ya serikali hazitekelezi “sera ya kuendelea” kwa wanaorudi- ambapo mwanafunzi mjamzito anaruhusiwa kuendelea kuwepo shule kwa kipindi anachoamua yeye mwenyewe. Vipindi virefu vya likizo ya uzazi, mchakato mrefu wa kurudi shuleni kama ule unaohitaji cheti cha matibabu kama vile Senegali au barua kwa baadhi ya maofisa elimu huko Malawi, au masharti magumu ambayo yanamtaka msichana kuomba kujiunga na shule tofauti, vyote hivi vinaweza kuathiri utayari wa mama kijana kurudi shuleni au uwezo wake wa kuendelea kujifunza.
Sababu nyingine nyingi zinachangia maelfu ya kina mama vijana kushindwa kuendelea na elimu rasmi. Kubwa zaidi ni kukosekana kwa uelewa juu ya sera za kurudi shuleni kwa jamii, wasichana, walimu, na maofisa wa shule kwamba wasichana wanaweza na wanapaswa kurudi shule. Wasichana wanaathirika zaidi na vikwazo vya kifedha, ukosefu wa msaada na uwepo wa ubaguzi wa hali ya juu katika jamii na shule.
Baadhi ya serikali zimejikita katika kupambana na vikwazo hivi pamoja na sababu zinazopelekea mimba za utotoni na kuacha shule, kwa kufanya yafuatayo kwa mfano:
- Kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanaweza kupata elimu sawa, na kuweka msaada wa kifedha kwa wasichana waliopo katika hatari ya kuacha shule kupitia mikakati ya elimu kwa wasichana kama ilivyo Kenya na Rwanda;
- Kutoa msaada wa kijamii na kifedha kwa kina mama vijana kama ilivyo Afrika Kusini;
- Kutoa huduma maalumu kwa kina mama vijana mashuleni, kwa mfano muda wa kunyonyesha au ruhusa watoto wanapoumwa au kwenda kliniki ya afya kama ilivyo Senegali;
- Kuwa na uwezekano kwa wasichana kuchagua zamu za asubuhi au jioni;
- Kuanzisha sehemu za watoto kucheza au vituo vya watoto wachanga karibu na shule kama ilivyo Gabon;
- Kutoa huduma ya ushauri mashuleni kwa wasichana wajawazito na kina mama vijana kama ilivyo Malawi; na
- Kuwezesha ufikiaji wa huduma za masuala ya mapenzi na afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na elimu sahihi ya masuala ya mapenzi mashuleni na katika jamii, na upatikanaji wa njia mbalimbali za kujikinga na kwa Afrika Kusini uwepo wa njia salama na halali za kutoa mimba.
Licha ya hatua hizi nzuri za nchi za Afrika, idadi kubwa bado inaweka sheria na sera ambazo moja kwa moja zinawabagua wasichana wajawazito na kina mama vijana katika elimu. Kwa mfano, Equatorial Guinea, Sierra Leone na Tanzania zinafukuza shule wasichana wajawazito na kuwanyima kina mama vijana haki ya kusoma katika shule za umma. Mara nyingi sera hizi hutokomeza nafasi za wasichana kurudi shuleni na kumuweka msichana na mtoto wake katika hatari ya ndoa za utotoni, ugumu wa maisha na manyanyaso. Kiuhalisia, wasichana hufukuzwa lakini sio wavulana waliowapachika mimba wasichana hata kama wao pia wako shuleni.
Human Rights Watch pia ilibaini kwamba nchi 24 za Afrika hazina sera za kurudi shuleni au sheria za kulinda haki za msichana mjamzito kupata elimu, jambo ambalo linapelekea utekelezaji usiokuwa na uwiano wa elimu ya lazima katika ngazi ya shule. Tuligundua kwamba nchi za Afrika Kaskazini kwa ujumla zinakosa sera zinazohusiana na kushughulikia mimba za wasichana mashuleni, lakini sambamba na hilo, wanaweka faini na adhabu kali kwa wasichana na wanawake ambao wanaripotiwa kushiriki au kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa. Nchi kama vile Morocco na Sudan, kwa mfano, zinatekeleza sheria za maadili ambazo zinaruhusu kuwashitaki kwa uhalifu wasichana kwa uzinzi, kukosa heshima au kushiriki ngono nje ya ndoa.
Nchi nyingine zinatumia njia hatarishi kutambua wasichana wajawazito na wakati mwingine kuwanyanyapaa na kuwadhalilisha hadharani. Wengine wanafanya vipimo vya lazima vya mimba kwa wasichana, ama kama sehemu ya sera rasmi ya serikali au mazoea binafsi ya shule. Vipimo hivi kwa kawaida hufanyika bila ridhaa ya wasichana na kukiuka haki zao za faragha na utu. Wasichana wengine huogopa udhalilishaji huo na kufikia kuacha shule wenyewe pale wanapogundua ni wajawazito, wakati wengine hufikia kutoa mimba kwa njia zisizo salama, hali ambayo inaweka afya na maisha yao hatarini.
Sera za serikali ambazo zinabagua wasichana kwa misingi ya ujauzito au ndoa zinakiuka wajibu wao wa kimataifa na kikanda wa haki za binadamu, na mara nyingi zinakinzana na sheria za nchi na haki za kikatiba na kudhoofisha ajenda ya maendeleo kitaifa.
Kuwaacha nyuma wasichana wajawazito na kina mama vijana ni hatari kwa maendeleo ya bara. Kutokumuacha yoyote nyuma kuna maanisha kwamba serikali za Afrika zinapaswa kurudia dhamira ya malengo ya maendeleo jumuishi na wajibu wa haki za binadamu kwa watoto wote, na kuhakikisha wanatekeleza sera zinazozingatia haki za binadamu kwa ngazi ya taifa na mitaa ili kulinda haki za wasichana wajawazito na kina mama vijana kupata elimu. Mimba za utotoni na zile za bahati mbaya zinahatarisha upatikanaji wa elimu kwa maelfu ya wasichana na kwa sababu hizi, serikali zinabidi kuzizuia kwa kuhakikisha taasisi za elimu zinatoa elimu, taarifa na ujuzi ili wasichana wajawazito na kina mama vijana waweze kufurahia haki zao za kuendelea na elimu.
Mapendekezo
Kwa Serikali zote za Umoja wa Afrika
Kuondoa mara moja Ubaguzi unaotokana na Ujauzito Shuleni katika Sera na Utendaji
- Komesha, katika sera na utendaji, ufukuzaji wa wanafunzi wa kike wanaopata mimba au kuolewa na kuweka mazingira mazuri shuleni kwa wanafunzi wajawazito na waliolewa.
- Komesha mara moja upimaji wa mimba shuleni.
- Kuhakikisha kesi za udhalilishaji wa kijinsia na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na madereva wa mabasi, walimu, au maofisa wa shule, zinaripotiwa kwa mamlaka husika za usimamizi, ikiwa ni pamoja na polisi, na kwamba kesi zinachunguzwa na kufikishwa mahakamani
Hakikisha Wanafunzi Wajawazito na Kina Mama Vijana Wanaweza kuendelea na Elimu
- Kupitisha haraka sera chanya za kujiunga tena na kuharakisha kanuni ambazo zinawezesha wasichana wajawazito na kina mama vijana walio katika umri wa kwenda shule kurudi shule za msingi na sekondari.
- Kuhakikisha wanafunzi wajawazito na walioolewa ambao wanatamani kuendelea na elimu yao wanaweza kufanya hivyo katika mazingira yasiyokuwa na unyanyapaa na ubaguzi, ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu wanafunzi wa kike kuchagua shule mbadala, na kufuatilia utii wa sheria hizi kwa shule.
- Kuwaunganisha wanafunzi wajawazito, walioolewa na wenye watoto na huduma za afya, kama vile zahanati za uzazi wa mpango.
- Kuanzisha mpango rasmi na rafiki, kama vile madarasa ya jioni au ya muda, kwa wasichana ambao hawana uwezo wa kuhudhuria masomo siku nzima, na kuhakikisha wanafunzi wanapata ithibati kamili na vyeti vya shule za sekondari wanapomaliza.
- Kuwaunganisha kina mama vijana katika mipango inayolenga wanafunzi wa kike walio katika hatari ya kuacha shule, na kuhakikisha mipango hiyo inajumuisha hatua za kutoa msaada wa kifedha kwa wanafunzi walio katika hali hatarishi, ushauri, ruzuku za shule, na usambazaji wa vifaa vya elimu na vya usafi, ikiwa ni pamoja na vifaa vihusianavyo na usafi wa hedhi katika shule.
- Kupanua wigo wa kuchagua huduma za mtoto na vituo vya maendeleo ya mtoto kwa ajili ya watoto wa kina mama vijana ili kwamba wasichana walio katika umri wa kwenda shule waweze kuhudhuria shule.
- Kuhakikisha kwamba misaada ya kibinadamu ya elimu katika maeneo ya vita au migogoro inajumuisha mahitaji maalumu ya wasichana wajawazito na kina mama vijana walio katika umri wa kwenda shule.
- Kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wazazi, walezi na viongozi wa jamii kuhusu madhara ya kimwili, kielimu, na kisaikolojia ya mimba za ujanani na umuhimu wa wasichana wajawazito na kina mama vijana kuendelea na shule.
- Kutoa huduma za ushauri shuleni kwa wanafunzi wajawazito, walioolewa, au kinamama. Kutoa msaada wa muda mrefu wa kisaikolojia kwa vijana walioathirika na unyanyasaji au udhalilishaji wa kingono.
- Kuwahusisha walimu na maafisa wengine wa elimu kuunga mkono elimu kwa msichana mjamzito na mama kijana, na kuhakikisha wanaweka mazingira salama shuleni.
- Kuboresha Takwimu na Kufuatilia Utekelezaji wa Sera za Shule kwa Wanafunzi Wajawazito. Shule zinapaswa:
- Kuboresha ufuatiliaji na ukusanyaji wa takwimu za wasichana wanaoacha shule kutokana na mimba au ndoa;
- Kuendeleza na kutekeleza mbinu za kufuatilia na kuweka kumbukumbu ya wasichana walioacha shule kutokana na mimba au ndoa, kwa lengo la kuanzisha utaratibu wa kuwarudisha shule;
- Kufuatilia utekelezaji wa sera za shule za kujiunga tena kwa kuweka takwimu za idadi ya wanafunzi wajawazito na waliiolewa ambao wanadahiliwa tena, mahudhurio yao shuleni na kiwango cha kumaliza; na kutumia taarifa hizo kuboresha msaada kwa wanafunzi wajawazito, walioolewa na kina mama.
Kuharakisha Mapambano ya Vikwazo Vinavyozuia Elimu kwa Msichana
- Kuhakikisha elimu ya msingi ni bure kiukweli kwa kuondoa ada, na kushughulikia upatikanaji wa elimu bure ya sekondari kama kipaumbele cha haraka badala ya lengo ambalo linaweza kufikiwa taratibu kwa kipindi fulani. Kuchukua hatua kushughulikia gharama zisizo za moja kwa moja za shule ya msingi na sekondari.
- Kuongeza umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 18 kwa wanaume na wanawake na kuchukua hatua zote za muhimu kuondoa ndoa za utotoni katika sheria na taratibu, ikiwa ni pamoja na kutekeleza mikakati ya kitaifa madhubuti na yenye ufanisi ya kupambana na ndoa za utotoni na kushirikishana mifano bora.
- Kutekeleza mipango ya kitaifa ya kumuwezesha msichana kwenda shule. Kubuni mipango mahsusi kwa jamii ambayo inaakisi mahitaji ya watoto na inalenga kujenga ujuzi wao katika mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na: ufahamu kuhusu masuala ya kijinsia na afya ya uzazi, usimamizi wa usafi wa hedhi, ufahamu wa ridhaa ya kushiriki ngono, ukatili wa kijinsia, na ndoa za utotoni, na utaratibu wa kuripoti unyanyasaji wa aina yoyote na kupata msaada.
- Kutekeleza kampeni ya taarifa kwa umma inayolenga familia, viongozi wa jamii, na vijana wa kiume na kike ambayo itagusia unyanyapaa wa mimba za utotoni, ngono na uzazi, na kujadili umuhimu wa elimu ya ngono na kuchochea njia za wazazi kuongea kuhusu ngono salama na ya afya.
Kuhakikisha Haki za Vijana za Uzazi na Ngono
- Kuongeza elimu ya lazima ya ngono na afya ya uzazi kama somo linalojitegemea, lenye mtihani katika mitaala ya shule za msingi na sekondari.
- Kuhakikisha kwamba mitaala ya lazima kitaifa ya masuala ya ngono inakubaliana na viwango vya kimataifa ambavyo ni:
- Ni pamoja na taarifa ya kina ya ngono na afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na taarifa ya haki za kijinsia na afya ya uzazi, tabia ya kuwajibika kuhusu kujamiiana na kujikinga na mimba za mapema na maambukizi ya magonjwa ya zinaa. Kuwa na taarifa na ujuzi unaohusiana na usawa wa kijinsia, uwezo wa kuwa na mahusiano yenye afya, ridhaa ya ngono na ndoa na kuweza kutofautisha, na kujikinga na udhalilishaji na ukatili wa kijinsia, pamoja na njia za kuripoti na kushughulikiwa;
- Ni ya lazima, inazingatia umri, na sahihi kisayansi;
- Inajumuisha mada zinazofaa kufundishwa shule za msingi; na
- Zinatoa taarifa kwa kushauriana na vijana.
- Kuwaandaa vyema waalimu kufundisha mtaala bila upendeleo.
- Kuhakikisha kwamba elimu na taarifa za ngono na afya ya uzazi zinapatikana kwa wanafunzi wenye ulemavu na zinapatikana katika mfumo rafiki kama vile vifaa maalumu kwa walemavu au katika muundo rahisi kusoma.
- Kupitisha sheria zinazoweka umri wa chini wa kuridhia kushiriki vitendo vya ngono na kupata huduma za kijinsia na afya ya uzazi, sawa kwa vijana wa kike na kiume, kwa kuzingatia taratibu za kimataifa za haki za binadamu na mifano bora.
- Kuhakikisha vijana wanaweza kupata huduma za afya katika maeneo wanayoishi ambazo pia ni rafiki kwa vijana na kuhakikisha wanaweza kufikia taarifa sahihi na njia zinazofaa za kujikinga na mimba za utotoni, VVU, na magonjwa ya zinaa. Ruhusa kutoka kwa mtu wa tatu ili kupata huduma hizi haipaswi kuwepo na nchi wananchama wanapaswa kujitahidi kuhakikisha kwamba uzazi wa mpango haulipiwi.
- Kuhakikisha kwamba vituo vya afya haviwatuhumu vijana ambao wanashiriki ngono, na kwamba wanakuwa na wafanyakazi waliohitimu kutoa huduma za afya na za siri kwa kina kwa vijana.
- Kuchukua hatua zote muhimu, za papo hapo na za kuendela, kuruhusu utoaji mimba na kuhakikisha kwamba wasichana na wanawake wana taarifa na kupata huduma za bure ambazo ni salama na zinakubalika kisheria za kutoa mimba kama kipengele cha kutumia haki yao ya uzazi na haki nyingine za kibinadamu.
Kwa Umoja wa Afrika
- Kuwataka nchi wanachama kuachana na ubaguzi juu ya ujauzito shuleni na unyanyasaji unaoendana na huu, pamoja na upimaji wa lazima wa mimba.
- Kufikiria kufanya kampeni ya bara zima kuunga mkono elimu kwa wasichana wajawazito, walioolewa na kina mama vijana. Kampeni hiyo ingeendeleza mafanikio ya Kampeni ya Kutokomeza Ndoa za Utotoni Afrika na Mpango Kazi wa Miaka Kumi wa Kijana wa Afrika, pamoja na mipango mingine ya kikanda ikiwa ni pamoja na Kampeni ya Kuharakisha Kupunguza Vifo vitokanavyo na Uzazi Afrika (CARMMA), Miaka Kumi ya Mwanamke wa Afrika na Mkakati wa Elimu kwa Bara la Afrika 2016 – 2025 (CESA 16-25).
- Kufanya utafiti wa kina wa sheria, sera na taratibu zilizopo ambazo zinaunga mkono au kuzuia elimu kwa msichana mjamzito au alieolewa au mama kijana kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, kwa lengo la kuwezesha njia iliyoratibiwa kiufanisi baina ya nchi na kushirikishana katika mienendo mizuri.
- Kuandaa mfano wa sera zinakubaliana na haki za binadamu za kuruhusu kujiunga tena na shule na miongozo kwa ajili ya serikali kuzifuata wakati wa kutengeneza sheria, sera au miongozo kuunga mkono elimu kwa msichana mjamzito, alieolewa au mwenye mtoto katika ngazi ya taifa na mtaa. Kuhimiza serikali kutekeleza sera zinazoruhusu wanafunzi wajawazito kuendelea kuwepo shule kwa kipindi wanachotaka, na sio kutoa likizo za lazima baada ya kujifungua.
Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Kamati ya Afrika ya Wataalamu wa Haki na Ustawi wa Mtoto
- Kutoa wito kwa serikali kufuta sheria na sera ambazo zinabagua wasichana wajawazito na kina mama vijana, ikiwa ni pamoja na sheria za jinai ambazo zimeweka adhabu kali za jinai kwa kufanya ngono nje ya ndoa.
- Kufuatilia utii wa serikali katika kutekeleza sera zinazounga mkono elimu kwa msichana mjamzito, alieolewa na mama kijana wakati wa ukaguzi wa serikali chini ya vyombo vya haki za binadamu.
Kwa Washirika wa Maendeleo na Mashirika ya Umoja wa Mataifa
- Kuhimiza nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kuzingatia wajibu wao kimataifa na kikanda juu ya haki za binadamu. Hasa kuhimiza na kuunga mkono serikali, kwa msaada wa kitaalamu na kifedha, kwa:
- Kukomesha, katika sera na utaratibu, kufukuzwa shule wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito au kuolewa na kusitisha mara moja upimaji wa mimba shuleni popote unapofanyika.
- Kuharakisha upitishwaji wa sera zinazozingatia haki za binadamu kuendelea au kujiunga tena na shule kwa wazazi walio katika umri wa kwenda shule. Kuhimiza serikali kutekeleza sera endelevu zinazoruhusu wanafunzi wajawazito kuendelea kuwepo shuleni kwa kipindi wanachotaka, na sio kutoa likizo za lazima baada ya kujifungua.
- Kuanzisha mitaala ya lazima juu ya elimu ya kina ya masuala ya ngono kwa shule za msingi na sekondari ambazo zinazingatia viwango vya kimataifa vya haki za binadamu; kutekeleza mitaala hii kama somo linalojitegemea na kufanyiwa mtihani.
- Kutoa msaada wa kitaalamu na kifedha kuwezesha utafiti wa kina kufanyika juu ya sheria, sera na taratibu zilizopo zinazounga mkono au kuzuia elimu kwa msichana mjamzito au alieolewa au mama kijana kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, kwa lengo la kuwezesha njia iliyoratibiwa kiufanisi baina ya nchi na kushirikishana katika mienendo mizuri.
- Kusaidia uaandaaji wa mfano wa sera zinakubaliana na haki za binadamu na miongozo kwa ajili ya serikali kuzingatia wakati wa kutengeneza sera au miongozo kuunga mkono elimu kwa msichana mjamzito, alieolewa au mwenye mtoto katika ngazi ya taifa na mtaa.
- Kuhakikisha elimu ya msingi ni bure kiukweli kwa kuondoa ada, na kushughulikia upatikanaji wa elimu bure ya sekondari kama kipaumbele cha haraka badala ya lengo ambalo linaweza kufikiwa taratibu kwa kipindi fulani. Kusaidia serikali kuchukua hatua kushughulikia gharama zisizo za moja kwa moja za shule ya msingi na.
Mbinu za Utafiti
Human Rights Watch ilifanya utafiti wa sheria, sera na taratibu zinazohusiana na wasichana wajawazito katika elimu kwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika. Tilipitia pia mikakati na ripoti za serikali katika sekta za elimu, afya na afya ya uzazi, tafiti za kitaaluma, uchambuzi wa sheria na taratibu uliofanywa na mashirika ya kitaifa na kimataifa katika mada hii pamoja na makala za magazeti.
Human Rights Watch iliwasiliana na wizara sita za elimu na/au wajumbe wa nchi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), ikiwa ni pamoja na Angola, Djibouti, Guinea ya Equatoria, Ivory Coast, Mali na Togo, kutafuta majibu rasmi ya sera na taratibu zinazotumika katika nchi hizi. Vile vile tuliwasiliana na asasi za kiraia za kitaifa na kikanda zinazoshughulikia elimu kwa wasichana na afya.
Ripoti hii inajumuisha shuhuda kutoka kwa wasichana wajawazito na kina mama vijana waliohojiwa na Human Rights Watch huko Malawi, Senegali, Tanzania na Zimbabwe. Ripoti hii pia inachukua taarifa zaidi kutoka katika tafiti za kina za Human Rights Watch juu ya haki za wasichana Afrika, ikiwa ni pamoja udhalilishaji unaohusiana na ndoa za utotoni, vikwazo vya elimu ya msingi na sekondari kwa wasichana, unyanyasaji wa kijinsia na ufikiaji wa haki za jinsia na afya ya uzazi.[1]
I. Historia: Mimba za Ujanani na Elimu ya Wasichana Afrika
Nilipata mimba mwaka jana nikiwa na umri wa miaka 14. Niliacha kwenda shule mwaka huo huo kwa sababu mama yangu … hakuweza kunipeleka shule. Nilikuwa na mahusiano na mtu mzima ambaye alikuwa na mke. Sikupata elimu ya masuala ya ngono kabisa, na nilipofanya mapenzi na huyo mwanaume nilipata mimba. Ninatamani kurudi shule kwani mimi bado ni mtoto.
—Abigail C., 15, Zimbabwe, Oktoba 2015
Mimba za Wasichana Vijana Afrika
Mimba za ujanani zimeongezeka kwa kiwango cha juu sana kusini mwa jangwa la Sahara Afrika, ambapo kuna kiwango kikubwa cha mimba za aina hiyo duniani.[2] Kila mwaka maelfu ya wasichana wa KiAfrika wanapata ujauzito wakati ambao walipaswa kuwa wanajifunza historia, aljebra, na stadi za maisha.[3] Wasichana wanaotoka katika kaya na jamii maskini ni miongoni mwa wanaoathirika zaidi.[4]
Sababu kubwa za mimba za ujanani Afrika ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na udhalilishaji, umaskini, ukosefu wa taarifa kuhusu ngono na uzazi, na ukosefu wa kufikia baadhi ya huduma kama vile mpango wa uzazi na uzazi wa kisasa.[5] Nyingi ya hizi mimba hazikupangwa na nyingi hutokea katika mazingira ya ndoa za utotoni, tatizo kubwa barani. Takribani asilimia 38 ya wasichana kusini mwa Jangwa la Sahara wanaolewa kabla ya miaka 18 na asilimia 12 kabla ya miaka 15.[6] Nchi za Afrika ni miongoni mwa nchi 15 kati ya 20 zenye kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni duniani.[7] Hata hivyo, bado serikali nyingi wanachama wa Umoja wa Afrika zimeshindwa kupitisha umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 18 kulinda wasichana dhidi ya udhalilishaji huu na kutetea haki zao za kupata elimu.[8]
Unyanyapaa juu ya Ngono za Vijana na Mimba Nje ya Ndoa
Katika nchi nyingi za Afrika, wahudumu wa elimu na afya mara nyingi wanawaaibisha, kuwanyanyapaa na wakati mwingine kuwatenga vijana wa kike wenye mimba za mapema na zile zisizotarajiwa.
Kulaumiwa na viongozi wa kisiasa au katika vyombo vya habari kunaweza kuhimiza na kuchochea unyanyapaa. Wasichana hao pia wanakabiliana na hatari kubwa ya unyanyasaji na vitendo vya kikatili au umaskini uliokithiri na ugumu wa uchumi.[9]
Linapokuja suala la elimu, baadhi ya serikali zinatumia hoja za maadili kuwatenga wasichana wajawazito na kina mama vijana. Kuwaruhusu kuendelea na shule, kwa mujibu wa hoja hiyo, kutafanya suala la kushika mimba nje ya ndoa kuwa la kawaida, kuwaondolea wasichana adhabu na kupelekea madhara zaidi ambapo wasichana wengi watashika mimba. [10] Hoja hizo hazina mashiko kutoka katika tafiti zozote za kuaminika.[11] Nchini Malawi, Senegali, Sudani Kusini na Tanzania, wasichana walioongea na Human Rights Watch walisema walikuwa na nia ya dhati kujiendeleza kielimu na tayari wanafahamu ugumu wa kuwa mama bila ya kuwekewa adhabu za ziada.
Ukosefu wa Taarifa na Elimu ya Ngono na Afya ya Uzazi kwa Vijana
Kuanzia umri mdogo, watoto wengi wanakutana na mawazo yanayopingana au hasi kuhusu ngono wakiwa nyumbani au hata shule. Katika kipindi cha kubalehe, familia, jamii na hata shule zinaweka matarajio ya kibaguzi ya majukumu, tabia na viwango vya maadili kwa wavulana na wasichana. Ijapokuwa mtazamo huo unaweza kuwazuia watoto wengi kuuliza maswali, kwa mujibu wa tafiti za UN za tabia za ngono za ujanani, mtazamo huo hauwazuii kujaribu: vijana wengi wana mahusiano ya kingono, mara nyingi kuanzia umri mdogo sana.[12] Wengi hufanya hivyo bila ya kuwa na taarifa muhimu wala kuwa na upatikanaji wa kutosha wa njia za kujikinga na mimba.[13]
Katika Umoja wa Afrika, serikali nyingi zimeshindwa kutekeleza elimu ya kina, sahihi kisayansi na yenye kuzingatia umri juu ya ngono na afya ya uzazi.[14] Hii inamaanisha kwamba wasichana na wavulana wengi wana uelewa finyu juu ya mabadiliko ya miili yao na tabia za hisia za kupevuka, jinsi ya kujikinga na mimba na magonjwa ya zinaa, mzunguko wa hedhi, elimu ya uzazi na unyanyasaji wa kingono na wa kijinsia.
Nchini Senegali na Tanzania kwa mfano, wasichana wengi waliohojiwa na Human Rights Watch hawakuwa wanajua kwamba wanaweza kushika mimba mara ya kwanza wanapofanya mapenzi.[15]
Nchi nyingine zinaendelea kufundisha kuepuka mahusiano ya kimapenzi kabla ya ndoa.[16] Ushahidi wa kisayansi, kijamii na haki za binadamu duniani unaonyesha kwamba mtaala wa kuepuka mahusiano ya kimapenzi haupelekei matokeo dhahiri kwa tabia za vijana waliopevuka kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi.[17] Mkazo mkubwa kwenye kujiepusha pia hutenga na kudhalilisha vijana wengi ambao tayari wameshashiriki ngono na kuwazuia kupata taarifa na huduma ambazo zinaweza kuwalinda na udhalilishaji, mimba zisizotarajiwa, au HIV na maambukizi mengine ya magonjwa ya zinaa.[18]
Aidha, ni nchi chache sana ambazo zimepitisha sheria zinazoweka wazi umri wa kuridhia kushiriki vitendo vya ngono.[19] Baadhi ya nchi bado zinaadhibu kujihusisha na ngono kwa ridhaa baina ya vijana waliopevuka, au mahusiano ya kingono nje ya ndoa.[20]
Kama sehemu ya juhudi zao juu ya haki za uzazi wa vijana, mashirika ya Umoja wa mataifa na vyombo vya kufuatilia mikataba ya haki za binadamu wameziomba serikali kuanzisha umri wa chini unaokubalika kisheria kujihusisha na ngono kwa ridhaa, kuweka uwiano wa ulinzi wa mtoto na uwezo wa ukuaji wake.[21] Kwa mujibu wa Kamati ya Haki za Mtoto ambayo inatoa ufafanuzi wa mamlaka juu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Mtoto, mataifa lazima yaweke “dhana ya kisheria kwamba vijana wana uwezo wa kutafuta na kupata kwa wakati huduma na bidhaa za kujikinga.” Pia ni muhimu kuepuka kuadhibu vijana wa umri sawa kwa kujihusisha na vitendo vya ngono ya ridhaa iliyothibitika na isiyokuwa ya kurubuniwa.[22]
Nchi nyingi za Umoja wa Afrika hazitoi huduma rafiki, zinazofikika na za siri kwa vijana juu ya masuala ya ngono na afya ya uzazi. Aidha, nchi nyingi za Umoja wa Afrika zinatoa adhabu kwa kutoa mimba, kitu ambacho kinamaanisha wasichana wenye mimba zisizotarajiwa ni lazima wabebe mimba hizo hadi mwisho bila matakwa yao, au kutafuta njia zisizo halali na mara nyingi zisizo salama za kutoa mimba.[23] Katika mabara yote duniani, Afrika ina idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na utoaji mimba usio salama.[24]
Vikwazo Vikuu vya Elimu kwa Msichana
Nina miaka 16, nilikimbia nyumbani na kwenda kuolewa nikiwa na miaka 14 baada ya kufanya mapenzi na mpenzi wangu, ambaye alikuwa na miaka 21. Nilikuwa naogopa familia yangu itajua kwamba nimefanya mapenzi, hivyo nilienda kuishi na mpenzi wangu kama mke wake. Nilikuwa darasa la saba wakati huo na niliacha kwenda shule. Baada ya miezi saba mume wangu na kaka zake watatu walianza kulalamika kwamba sipati mimba. Hakuwa ananipiga lakini alikuwa akilalamika kila wakati kwamba mimi ni tasa. Nilikuwa nikifanya kazi nyingi ngumu kama kufua nguo, kufanya usafi na kupika kwa ajili ya mume wangu na ndugu zake. Baada ya miaka miwili ya ndoa, alinifukuza akidai kwamba mimi ni tasa, na mama yangu alinipokea. Natamani kurudi shule lakini mama yangu hana uwezo wa kunipeleka shule.
—Munesu C., 16, Zimbabwe, Oktoba 2015
Barani Afrika, wasichana wanakabiliwa na changamoto za kipekee katika kupata elimu kutokana na kutokuwepo na usawa wa kijinsia na kimuundo. Pamoja na juhudi za serikali, bado kumeendelea kuwepo tofauti kubwa za kijinsia katika fursa za elimu na mapungufu ya wazi ya kijinsia katika mafanikio ya na kujifunza stadi mbalimbali.[25]
Vikwazo vya elimu kwa msichana ni vingi na vinaingiliana, lakini serikali chache za Afrika zimeshughulikia mambo muhimu yanayopelekea mamilioni ya wasichana kuacha shule, ikiwa ni pamoja na:
- Gharama kubwa ya ada pamoja na gharama zisizokuwa za moja kwa moja za kuhudhuria shule za msingi na sekondari[26];
- Mazingira ya shule yasiyo salama ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, udhalilishaji na kurubuniwa na walimu, maafisa wa shule na wanafunzi wengine; unyanyapaa unaohusishwa na mimba na kuolewa; adhabu za viboko zitolewazo na walimu na maafisa wa shule ambazo wakati mwingine zinakiuka ubinadamu; na umbali mrefu kwenda shule kwa maeneo ya vijijini ambao unamuweka msichana katika hatari ya ukatili wa kijinsia na hatari nyinginezo[27];
- Ubaguzi unaofanywa na walimu na maafisa wa shule na kukosekana kwa miundombinu wezeshi kwa wasichana wenye ulemavu[28];
- Miundombinu mibovu ikiwa ni pamoja kukosekana kwa maji ya kutosha na vyoo, na maji yanayotoka bombani ili kukidhi mahitaji kipindi cha hedhi[29]; na
- Mila potofu na ukosefu wa usawa wa kijinsia ambao hauungi mkono elimu kwa wasichana na wanawake, ubaguzi na utamaduni kama vile ndoa za utotoni.[30]
Mimba ni kikwazo kwa msichana kuendelea na shule na mara kadhaa hupelekea wasichana kuacha shule. Tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba kukaa muda mrefu shule kwa msichana kunapunguza uwezekano wa kuolewa akiwa mtoto na/au kupata ujauzito akiwa na umri mdogo.[31]
II. Elimu kwa Wasichana Wajawazito na Kina Mama Vijana: Wajibu wa Serikali wa Haki za Binadamu
Serikali za Afrika zinabanwa na sheria za kimataifa za haki za binadamu kutoa elimu ya lazima ya msingi bure na kuhakikisha elimu ya sekondari inapatikana na inafikika na wote bila ubaguzi. [32] Haki ya kupata elimu ya sekondari inajumuisha “kukamilisha elimu ya msingi na kuimarisha misingi ya kujifunza bila kikomo na maendeleo ya binadamu.”[33]
Human Rights Watch imezitaka serikali duniani kote kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kwamba elimu ya sekondari inapatikana na kufikika na wote bila malipo. Inaeleweka kwamba serikali nyingi za Afrika na maeneo mengine zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa rasilimali ambao hupunguza uwezo wao wa kufikia mara moja malengo muhimu ya haki za binadamu kama vile elimu bure ya sekondari kwa wote. Hata hivyo Human Rights Watch inaamini kwamba ni muhimu kwa serikali kuchukulia upatikanaji wa elimu bure ya sekondari kama jambo la kipaumbele cha haraka badala ya lengo la kufikiwa hatua kwa hatua kwa muda mrefu.
Katika ngazi ya kikanda Afrika, Umoja wa Afrika umepitisha mfumo wa kisheria ambao unalinda haki ya elimu kwa wasichana wote. Nchi zote za Afrika kasoro saba zimekubaliana na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa mtoto, ambao unazitaka serikali kuchukua hatua maalumu kuhakikisha ufikiaji sawa wa elimu kwa wasichana, kuongeza umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 18, na kuchukua hatua zote stahiki kuhakikisha wasichana wanaopata mimba kabla ya kumaliza elimu yao wanakuwa na haki ya kuendelea na elimu.[34]
Mkataba wa Vijana Afrika-uliopitishwa na zaidi ya nusu ya serikali za Afrika-unawajibisha serikali kuhakikisha wasichana na wanawake vijana wanaopata mimba au kuolewa kabla ya kumaliza masomo yao kuwa na fursa ya kuendelea na masomo yao.[35] Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Kamati ya Afrika ya Wataalamu wa Haki na Ustawai wa Mtoto wameomba mataifa kuweka hatua za kupeleka watoto wote shuleni, kuweka hatua za kufikia upatikanaji sawa wa elimu kwa wasichana na wavulana, na kuhamasisha wasichana wajawazito kuhudhuria au kurudi shuleni. Vyombo hivi kwa pamoja vimesema kuwa, “ni lazima… kuwezesha uhifadhi na kuwarudisha shuleni wasichana wajawazito au walioolewa… na kuendeleza mipango ya elimu mbadala… katika mazingira ambayo wanawake hawawezi au hawako tayari kurudi shuleni baada ya ujauzito au ndoa.”[36]
Itifaki ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Haki za Wanawake, pia unajulikana kama Mkataba wa Haki za Wanawake Afrika, unatoa wajibu mahususi kuhakikisha haki za masuala ya jinsia na afya ya uzazi kwa wasichana.[37] Hii ni pamoja na haki ya kupata huduma ya kutoa mimba inapotokea udhalilishaji wa kingono, ubakaji, au pale mimba inapohatarisha afya ya akili, mwili na maisha ya mama.[38]
III. Mimba za Utotoni na Kutengwa katika Elimu kwa Umoja wa Afrika
Kulikuwa na mwalimu wa masomo ya ziada [binafsi] ambaye alikuwa akinifundisha mimi binafsi. Nilinyanyaswa kingono na mwalimu huyo hadi nikapata ujauzito. Baada ya kugundua ni mjamzito, nilimwambia mwalimu na akatoweka. Ndoto yangu ilizimwa kipindi hicho. Nilifukuzwa shule. Nilifukuzwa nyumbani pia. Nilienda kuishi na rafiki yangu mpaka nilipojifungua. Nilimlea mwanangu peke yangu kwa kujishughulisha na biashara ndogo ndogo. Mpaka hivi sasa.
—Imani, 22, Mwanza, Tanzania, Januari 2016
Idadi kubwa ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wamepitisha sheria na sera zinazolinda haki ya msichana kubaki shule kipindi cha ujauzito na kipindi cha kulea. Nchi hizi zinaweza kutumika kama mfano kwa nchi nyingine nyingi ambazo hazina sera za kutosha, na hasa kushawishi nchi chache ambazo zimepitisha au kuhamasisha hatua za adhabu na ubaguzi dhidi ya kina mama vijana kupitisha sera za kuzingatia haki za binadamu. Ingawa ni vyema kutambua kuwa serikali nyingi zinachagua kuwabakiza kina mama vijana shuleni, sheria na sera zao hazitimizwi kikamilifu, na ufuatiliaji wa kina mama vijana kurudi katika elimu umebaki kuwa dhaifu kwa ujumla.
Nchi zenye Sera za Kuendelea au Kujiunga tena
Nchi 26 wananchama wa umoja wa Afrika wana sheria, sera au mikakati ya kuhakikisha haki za msichana kurudi shuleni baada ya ujauzito.[39]
Katika kundi la nchi hizi, sita zina sheria zinazowaruhusu wasichana kuendelea na elimu yao.[40]
Hata hivyo, ukosefu wa sera zinazoelezea mchakato wa kufuatwa na shule ili kuwezesha wasichana kuendelea baada ya ujauzito mara nyingi husababisha wasichana kufukuzwa shule.[41]
Nchi zenye sheria za kitaifa zinazohusiana na haki ya elimu kwa wasichana wajawazito na kina mama |
|
Benin |
Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo |
Lesotho |
Mauritania |
Nigeria |
Sudan Kusini |
Nchi nne zina sera au mikakati inayoruhusu “kuendelea:” wanaruhusu msichana mjamzito kubaki shuleni, na hawahitaji kutokuwepo kwa lazima baada ya kujifungua.[42]
Nchi zenye sera au mikakati inayoruhusu “kuendelea” |
|
Cape Verde |
Gabon |
Ivory Coast |
Rwanda |
Nchi kumi na tano zina sera ya kurudi shule yenye masharti ambayo humtaka msichana mjamzito au mama kijana kuacha shule lakini kutoa fursa ya kurudi iwapo watatekeleza masharti kadhaa.[43] Sera ya kurudi shule zinataka kwamba mwanafunzi aache shule anapopatikana kuwa na ujauzito. Wakati mwingine, ikiwa mtu anayehusika na ujauzito ni mwanafunzi katika shule hiyo atahitajika kuchukua likizo ya kutokuwepo shuleni.[44] Msichana anaweza kudahiliwa-wakati mwingine katika shule tofauti baada ya kujifungua.[45] Sera na taratibu hutofautiana hususan kuhusu urefu wa muda ambao msichana anaruhusiwa kutokuwepo shuleni na utaratibu wa kujiondoa au kujiunga tena.[46]
Nchi zenye sera ya “kujiunga tena” ambazo zimeweka masharti kwa mama kijana |
|
Botswana |
Burundi |
Cameroon |
Gambia |
Kenya |
Liberia |
Madagascar |
Malawi |
Msumbiji |
Namibia |
Senegali |
Afrika Kusini |
Swaziland |
Zambia |
Zimbabwe |
Baadhi ya masharti ya kujiunga tena ni magumu kwa wasichana kuyafikia.[47] Wakati mwingine masharti huwa magumu au hayaeleweki, au yanahusisha maelekezo yenye madhara kama vile upimaji mimba kwa lazima.[48] Kwa mfano, nchini Malawi wasichana husimamishwa mara moja wanapogundulika kuwa wajawazito kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini wanaweza kudahiliwa tena mwanzo wa mwaka unaofuata wa elimu baada ya kusimamishwa kwao. Mama kijana anaetaka kuomba tena kudahiliwa lazima atume maombi mawili: moja kwa Wizara ya Elimu na moja kwa shule anayotaka kwenda.[49] Nchini Senegali, mama kijana ni lazima awasilishe cheti cha matibabu kuonyesha kwamba ana afya na yuko tayari kuendelea na masomo ili aweze kupata udahili.[50]
Mbali na sera zao za kujiunga tena, baadhi ya serikali hizi zimeshughulikia vikwazo vya moja kwa moja kwa mama kijana anayerudi shule, kwa mfano:
- Kuondoa ada za shule za msingi na sekondari na gharama zisizokuwa za moja kwa moja;
- Kutoa upendeleo maalumu kwa mama kijana aliye shule, kwa mfano muda wa kunyonyesha au kumruhusu msichana kupata mapumziko wakati mtoto anapoumwa[51];
- Kutekeleza mpango rafiki wa kujifunza, kama vile kumpa fursa msichana kuhudhuria madarasa ya asubuhi au jioni[52];
- Kutoa msaada wa kijamii na kifedha kwa mama kijana[53];
- Kuanzisha vituo vya watoto karibu na shule za sekondari[54]; na
- Kutoa huduma ya ushauri shuleni kwa wasichana wajawazito na/au kina mama vijana.[55]
Senegali: Kuunga mkono Kujumuishwa kwa Kina Mama Vijana
Mwaka 2007, Senegali ilipitisha waraka wa “usimamizi wa ndoa na ujauzito mashuleni,” ambao unaziagiza shule kuwasimamisha wasichana kuendelea na elimu kwa muda mpaka watakapojifungua, kwa sababu za kiusalama. Ili kurudi shule, wasichana ni lazima waonyeshe cheti cha matibabu ambacho kinaonyesha kwamba wako tayari kurudi shule. Wasichana wanaweza kupata vyeti hivi wanapohudhuria zahanati za afya au hospitali.
Kiuhalisia, Human Rights Watch iligundua kwamba wasichana huruhusiwa kuendelea na shule mpaka wanaposhindwa kuhudhuria, ijapokuwa baadhi ya shule huwasimamisha wasichana katika mwezi wa sita au wa saba wa ujauzito. Wasichana wajawazito au kina mama vijana pia wanaweza kufanya mitihani. Mkurugenzi katika mji wa kusini wa Vélingara anasema kwamba kuwasaidia wasichana wajawazito ni muhimu kuhakikisha wanarudi pale wanapokuwa tayari kuendelea na elimu yao: “ Kuna uelewa kati ya wafanyakazi kwamba kama wao [kina mama vijana] wanachelewa, au hawahudhurii kwa sababu ya watoto wao, tunawaelewa. [Pia tunatoa nafasi] kwa wasichana wajawazito wanaosinzia darasani, au wale wanaoomba chakula kwa sababu wana njaa.”
Fatoumata, 17, anaishi Sédhiou na anahudhuria shule ya sekondari mjini hapo. Alipata ujauzito alipokuwa na miaka 16 na aliruhusiwa kubaki shuleni. Mwezi mmoja baada ya kujifungua, aliendelea kwenda shule. Bibi yake alimlea mtoto wake. “Sikutaka kupata mtoto,” Fatoumata aliwaambia Human Rights Watch. “Nimewaeleza rafiki zangu wote wasijaribu kupata mtoto… inasababisha matatizo mengi… Lakini ikitokea umepata mtoto, ni lazima urudi shule baada ya kujifungua. Hakuna haja ya kuona aibu. Kukosea ni ubinadamu.” Fatoumata hakufundishwa kuhusu ngono na afya ya uzazi shuleni. “Ingesaidia sana kupata taarifa za njia za kujikinga na mimba,” alisema.
Human Rights Watch iligundua kwamba katika baadhi ya shule za Senegali, walimu wanaweka mkazo katika kujiepusha na kutunza bikra kabla ya ndoa. Baadhi ya shule huwa na vilabu vya majadiliano na kuzungumza na wanafunzi kuhusu njia za uzazi wa mpango, na kujikinga na mimba, VVU na magonjwa ya zinaa. Human Rights Watch iligundua kwamba katika baadhi ya vilabu, wasichana hudanganywa kwamba vidonge vya uzazi wa mpango ni vibaya kwa wasichana ambao hawajaolewa kwa sababu vinapunguza uwezekanao wao wa kushika mimba au vinaweza kupelekea kwa kichanga kufariki kipindi cha kujifungua.
Mara nyingi, usambazaji mbovu katika ngazi za shule na ukosefu wa uelewa wa sera hizi kwa walimu, jamii, na wasichana wenyewe hupunguza ufanisi wake.[56] Kwa mfano, maafisa wa shule hawajitoi kufuatilia wasichana walioacha shule kutokana na ujauzito ili kuwawezesha kurudi shuleni. Kwa kiasi kikubwa takwimu zinakosekana za idadi ya wasichana wanaoacha shule kutokana na ujauzito; kina mama vijana wanaodahiliwa katika shule kwa kufuata sera hizi; changamoto wanazokutana nazo baada ya kudahiliwa; na, na maendeleo yao baada ya kurudi shuleni.[57]
Nchi nyingine zimehama kutoka sera za kuzuia na hata zile zinazotoa adhabu na kutoa fursa kwa wasichana kuendelea.[58] Mwaka 2017, kwa mfano, Cape Verde ilibadilisha sera yake ya kufukuza, na kuwapa wanafunzi wajawazito likizo ya uzazi, na kudhamiria kuhakikisha mazingira mazuri katika shule zenye kina mama vijana.[59]
Wakati wa uandishi, nchini Ghana na Uganda, serikali na asasi za kiraia zilikuwa zikijadili sera za kujiunga tena au miongozo ya elimu kwa kina mama vijana.[60]
Nchi zilizoathirika na vita vya silaha huwa na viwango vikubwa vya mimba kutokana na, kwa kiasi fulani, kuenea ukatili wa kingono unaofanywa na wanachama wa viko vya kitaifa vyenye silaha na vikundi vyenye silaha, na kiwango kikubwa cha umaskini ambacho kinawezesha unyanyasaji wa kingono. Nchi hizi zinahitaji sera zenye nguvu za kurudi shule. Hali za migogoro zinaongeza ukosefu wa usawa wa kijinsia na ubaguzi wa kijinsia, ambao tayari upo katika nchi nyingi zilizo katika migogoro. Baadhi ya waathirika wa ukatili wa kingono hawarudi shuleni kwa sababu ya unyanyapaa na unyonge, na wale wanaorudi shule hukosa msaada wa kuendela na elimu yao.[61] Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini, kwa mfano, zina sheria ambazo hulinda haki za kina mama vijana kurudi shule.[62] Kwa upande mwingine, Human Rights Watch iligundua kuwa Jamhuri ya Afrika ya Kati haina sheria wala sera zinazolenga kusaidia.[63]
Human Rights Watch iligundua kwamba utafiti wa mahitaji ya elimu na ushughulikiwaji wa migogoro ya kibinadamu mara chache humuhusisha msichana mwenye mtoto.[64] Kushindwa kuhudumia mahitaji ya elimu ya mama kijana, pamoja na wale waathirika wa ubakaji, katika mazingira ya kibinadamu sio tu huzuia upatikanaji wa elimu bali pia huwaweka watoto walioko katika hali hatarishi katika hatari zaidi, ugumu na umaskini.
Nchi Zinazotenga Kina Mama Vijana
Serikali chache wanachama wa Umoja wa Afrika wameendelea kuwatenga wasichana wajawazito kupata elimu. Wawakilishi waandamizi wa serikali katika nchi kama vile Guinea ya Equatoria, Sierra Leone, na Tanzania wametangaza hadharani kwamba wasichana wajawazito wanapaswa kufukuzwa shule za umma.[65]
Katika nchi hizi, mara kadhaa wanasiasa wamehimiza hatua za adhabu kuwekwa kwa wasichana wanaowashutumu kwa “kukosa maadili”.[66] Nchini Tanzania, maafisa wa serikali na polisi wamefikia hatua ya kuwakamata wasichana wajawazito na kulazimisha familia zao kutaja majina ya wahusika waliowapa ujauzito.[67] Wasichana wengi waliohojiwa na Human Rights Watch ambao wameacha shule au kufukuzwa kutokana na ujauzito au ndoa walionyesha kujutia kushindwa kuendelea na elimu yao.[68]
Ijapokuwa Togo imetangaza kwa taasisi za Umoja wa Mataifa kwamba haifuati tena sheria inayokataza wasichana wajawazito kwenda kwenye vituo vya elimu, haijaondoa rasmi sheria hiyo au kuibadilisha kwa kuweka sera chanya ya kuendelea au kujiunga tena na elimu.[69]
Tanzania: Sera za Kibaguzi Dhidi ya Wasichana Wajawazito na Kina Mama Vijana Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Kamati ya Afrika ya Haki na Ustawi wa Mtoto, na Mwandishi Maalumu wa Tume ya Afrika juu ya Haki za Wanawake Afrika, kati ya wengine, wameitaka serikali ya Tanzania kusitisha marufuku yake ya kibaguzi dhidi ya wasichana wajawazito. Wataalamu wa Haki za binadamu wameitaka serikali kuhakikisha wasichana wajawazito na kina mama vijana wanaweza kurudi kuendelea na elimu katika shule za umma.[70] Kabla ya Rais John Magufuli kupiga marufuku hadharani mwaka 2017 kwa wasichana wajawazito na kina mama vijana kuwepo mashuleni, maafisa waandamizi wa elimu serikalini walikuwa tayari wanaamini wasichana wajawazito hawapaswi kuwepo shuleni na wanaweza kuleta ushawishi mbaya kwa wasichana wengine, kwa kufanya ujauzito shuleni kuwa jambo la “kawaida”.[71] Kufukuzwa kwa wasichana wajawazito shuleni kunaruhusiwa chini ya kanuni za elimu Tanzania, ambazo zinasema kwamba “mwanafunzi anaweza kufukuzwa shule pale … mwanafunzi anapokuwa … ametenda kosa kinyume cha maadili” au “ameingia kwenye ndoa.” [72] Sera hii haielezi makosa ya uvunjifu wa maadili ni yapi, lakini maafisa wa shule mara nyingi wanatafsiri suala la kubeba mimba kama mojawapo ya makosa hayo. Maafisa wa shule za sekondari mara kwa mara wanawafanyia wasichana vipimo vya mimba vya lazima kama hatua za kinidhamu za kuwafukuza shule wasichana wenye ujauzito. Kuanzia mwaka 2018, serikali imekuwa ikiandaa miongozo mipya ambayo itatoa muongozo wa kuingia katika mfumo rasmi uliopo wa elimu ya msingi ya umma kwa kina mama vijana, sawa na mpango uliopo wa kufuatilia watoto waliopo nje ya shule. Human Rights Watch waligundua kwamba mfumo huu ni duni, unakuja na gharama kubwa kwa wanafunzi na hauwawezeshi wanafunzi kupata ujuzi sawa au kuwapatia ithibati sawa. Wanafunzi wanaopitia mfumo huu hulipa ada inayofikia shilingi 500,000 za Kitanzania (US$227) kwa mwaka, ambapo wanafunzi wa shule za umma hawalipi ada au gharama zisizo za moja kwa moja. Upatikanaji wa mafunzo bora ya ufundi stadi yanatolewa katika baadhi tu ya vyuo nchini. Zaidi ya hapo, vijana wanaoacha shule za sekondari kabla ya wakati wanakosa ithibati na masomo yanayotakiwa ili kuendelea na elimu rasmi ya ufundi stadi na shahada ya mafunzo ya ujuzi.[73] |
Nchi Zinazokosa Sera za Wazi
Nchi ishirini na nne hazina sera za kujiunga tena au sheria za kulinda haki ya msichana mjamzito kupata elimu, ikiwa ni pamoja na angalau nchi sita ambazo ni uvunjifu wa sheria kufanya ngono nje ya ndoa. [74] Mara nyingi hali hii hupelekea usimamizi unaokosa uwiano wa elimu ya msingi katika ngazi ya shule, ambapo maafisa wa shule wanaweza kuamua hatma ya elimu ya msichana mjamzito. Nchini Burkina Faso, kwa mfano, maafisa wa serikali wamepitisha mkakati wa kuzuia mimba za utotoni, lakini maafisa wa shule mara nyingi huzuia wasichana wajawazito kuhudhuria shule kwa sababu ya desturi zenye nguvu katika jamii pamoja na unyanyapaa uliowekwa kwa kupata watoto nje ya ndoa.[75] Nchini Angola, kwa mfano, wasichana wajawazito huombwa kuhamia shule za usiku.[76]
Nchi Zinazokosa Sera za Wazi au Sheria |
||
Angola |
Burkina Faso |
Jamhuri ya Afrika ya Kati |
Chad |
Comoros |
Djibouti |
Ethiopia |
Eritrea |
Ghana |
Guinea |
Guinea-Bissau |
Mauritius |
Niger |
Jamhuri ya Kongo |
São Tomé e Príncipe |
Shelisheli |
Somalia |
Uganda |
Nchi ambazo Ngono Nje ya Ndoa ni Uhalifu
Human Rights Watch iligundua kuwa nchi za Afrika ya kaskazini kwa ujumla hazina sera zinazohusiana na namna ya kushughulika na ujauzito wa wasichana shuleni, lakini wakati huo huo zinaweka adhabu kali kwa wasichana na wanawake ambao wanaripotiwa kujihusisha na mahusiano ya ngono nje ya ndoa.[77] Nchi kama vile Morocco na Sudan, kwa mfano, zinatekeleza “sheria za maadili” ambazo zinawaruhusu kuwashtaki wasichana waliopevuka au wanawake na kuwatia hatiani kwa uzinzi, kukosa heshima au ngono nje ya ndoa.[78] Wasichana na wanawake wadogo wenye watoto, ambao mara kadhaa wanaonekana kama wameleta aibu kwenye jamii zao, wanadhihakiwa hadharani, kutengwa na kufungwa gerezani, na hawatarajiwi kuendelea na shule.[79]
Usimuache Kijana wa Kike Nyuma? |
|||||
Nchi zenye sera au amri za kufukuza |
Nchi zenye sera za masharti ya “kurudi” |
Nchi zenye sera au mikakati inayoruhusu “kuendelea” |
Nchi zenye sheria zinazolinda haki za wasichana wajawazito kubaki shule au kurudi kwenye elimu lakini zinakosa sera |
Nchi zenye sheria au taratibu zinazowaadhibu wasichana na wanawake wanaopata ujauzito nje ya ndoa |
Nchi zisizokuwa na sheria au sera zinazohusiana na kuwabakisha shule wasichana wajawazito au kina mama vijana shule |
Guinea ya Equatoria Sierra Leone Tanzania Togo |
Afrika Kusini Botswana Burundi Cameroon Gambia Kenya Liberia Madagascar Mali Malawi Msumbiji Namibia Senegali Swaziland Zambia Zimbabwe |
Cape Verde Gabon Ivory Coast Rwanda |
Benin Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo Lesotho Mauritania Nigeria Sudan Kusini |
Algeria Libya Misri Morocco/ Sahara Magharibi Sudan Tunisia |
Angola Burkina Faso Chad Comoros Djibouti Eritrea Ethiopia Ghana Guinea Guinea-Bissau Jamhuri ya Afrika ya Kati Jamhuri ya Kongo Mauritius Niger São Tomé na Príncipe Shelisheli Somalia Uganda |
IV. Kufungua Milango ya Shule kwa Wasichana Vijana Wote
Ujauzito na uzazi ni matukio makubwa ambayo hubadili maisha, zaidi sana kwa wasichana vijana. Kupitia hali hii wangali shuleni-huku pakiwa na unanyanyapaa au kukataliwa, kukosa msaada au kuupata mdogo kutoka kwa familia au shule, kulaumiwa na maafisa wa serikali, kukabiliana na ugumu wa kiuchumi na wakati mwingine ukatili na kudhalilishwa- kunaweza kupelekea changamoto kubwa kwa wasichana wajawazito na kina mama vijana kuendelea na elimu yao.
Hata hivyo, badala ya kuwapa majina wasichana wajawazito na kina mama vijana kama wakiukaji wa “maadili”, kuwaadhibu na kuwatenga shule, serikali za Afrika zina wajibu chini ya sheri za kimataifa za haki za binadamu kuhamasisha na kusaidia elimu na maendeleo ya taaluma kwa wasichana hawa bila ubaguzi.
Kwa ujumla, mbinu madhubuti zinahitajika kupunguza mimba za mapema na zisizotarajiwa kwa vijana na kuwasaidia kina mama vijana kuendelea na elimu. Utaratibu mzuri barani kote unaonyesha kuwa sekta ya elimu ina nafasi ya kipekee kushughulikia mimba za utotoni, ikiwa ni pamoja na kushughulikia baadhi ya sababu zake za msingi na kukabiliana na athari za elimu, afya na jamii na mahitaji ya msichana mjamzito na mama kijana.
Nchi za Umoja wa Afrika zinazo heshimu sera na utaratibu mzuri zimezingatia kwa uchache hatua zifuatazo: kuuunga mkono wasichana kubaki shuleni kwa kuondoa ada za shule ya msingi na sekondari kuhakikisha wanafunzi wote wanaweza kupata elimu sawa; kutoa msaada wa kifedha kwa wasichana walio katika mazingira magumu na hatarishi; kuhakikisha shule ni salama kwa wanafunzi kwa kuhakikisha shule zina taratibu zinazo jitosheleza za ulinzi kwa mtoto; kuwapatia vijana huduma za masuala ya kijinsia na afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na elimu ya kina ya masuala ya ngono shuleni na katika jamii; na kuhakikisha upatikanaji wa mbinu mbalimbali za kuzuia mimba, na utoaji mimba salama na unaofuata sheria .[80]
Shule ni lazima zihakikishe uhusishaji wa wanafunzi wote na kuchukua hatua madhubuti kulinda watoto dhidi ya unyanyasaji wa kingono, kurubuniwa, au kudhalilishwa. Shule pia zina jukumu la muhimu la kuwapatia wanafunzi taarifa na zana ili kuelewa mabadiliko yatokanayo na kupevuka, jinsia, na uzazi, na kuwapa taarifa zitakazo wawezesha kufanya maamuzi sahihi, bila shinikizo, kubaguliwa au dhana za uongo kutoka kwa marafiki au jamii.
Serikali zinapaswa kupitisha mitaala ya lazima kitaifa kwa shule ambayo itahusisha jinsia na afya ya uzazi na haki, tabia ya makini kuhusu kujamiiana, kuanzisha mahusiano sahihi, kujikinga na mimba za mapema na ndoa, kujikinga na magonjwa ya zinaa, usawa wa kijinsia, na ufahamu na kujikinga na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.[81] Muongozo wa ushahidi wa kitaalamu unaonyesha kwamba watoto wanapaswa kutambulishwa maudhui ya jinsia na afya ya uzazi yanayofaa kulingana na umri wao wakiwa shule za msingi, kabla ya kupevuka.[82]
Shukrani
Ripoti hii imeandikwa na Elin Martínez, mtafiti katika Idara ya Haki za Watoto Human rights Watch, na Agnes Odhiambo, mtafiti mwanadamizi katika Idara ya Haki za Wanawake. Utafiti katika ripoti hii ulifanywa na Elin Martínez, kwa usaidizi kutoka kwa Allison Cowie, Aurélie Edjidjimo Mabua na Elena Bagnera, wanafunzi wa vitendo wa haki za Watoto, Ochieng Angayo, mtafiti msaidizi, na Leslie Estrada, Mshirika wa Haki za Watoto.
Ripoti imehaririwa na Zama Neff, Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Haki za Watoto. James Ross, mkurugenzi wa Sheria na Sera, na Babatunde Olugboji, naibu mkurugenzi wa mipango, alietoa maoni ya kisheria na mipango. Margaret Wurth, mtafiti wa Haki za Wanawake na Haki za Watoto; Corinne Dufka, Mkurugenzi mshirika wa Afrika Magharabi; na Mausi Segun, Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Afrika, alietoa maoni ya kitaalamu. Ripoti pia imepata maoni kutoka kwa watafiti katika idara za Afrika, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Dr. Chi-Chi-Undie, wa Baraza la Idadi ya Watu, alifanya mapitio kama mtaalamu wa nje. Msaada wa uzalishaji ulifanywa na Leslie Estrada, mshirika wa Haki za Watoto; mshirika wa picha na machapisho; na Fitzroy Hepkins, meneja wa utawala.
Tunapenda kuwashukuru wataalamu kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali ya kitaifa na kimafaita, wizara za elimu na mashirika ya Umoja wa Mataifa ambao wametusaidia kufanya utafiti katika ripoti hii, na kushirikiana nasi kwa kutupa takwimu na taarifa nyingine. Wataalamu na wawakilishi hao ni pamoja na: Van Daniel wa Pairs Educateurs et Promoteurs sans Frontieres nchini Cameroon, Nicolas Effimbra wa Wizara ya Elimu ya Ivory Coast, Najlaa Elkhalifa, Bernard Makachia wa Elimu kwa Maisha Bora, Sabrina Mahtani wa Amnesty International, Trine Petersen wa UNICEF Lesotho, Ndiaye Khadidiatou Sow wa Wizara Elimu ya Taifa Senegali, na Boaz Waruku wa Mtandao wa Kampeni Afrika wa Elimu kwa Wote. Pia tunapenda kumshukuru Dr. Chi-Chi Undie wa Baraza la Idadi ya Watu kwa kutoa maoni ya kitaalamu, na Françoise Kpeglo Moudouthe, wa Wasichana sio Wake, kwa ushauri wa kimkakati.