- Mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa Rapid Support Forces na wapiganaji wengine pale El Geneina, mji mkuu wa eneo la magharibi mwa nchi hiyo la Darfur yameua angalau maelfu ya watu na kuacha mamia ya maelfu wakiwa wakimbizi.
- Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya watu wa jamii ya Massalit na jamii nyingine zisizokuwa za Kiarabu kwa nia ya kuwaondoa kabisa katika eneo hilo ni sawa na ufurushaji wa kikabila.
- Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika lazima kwa dharura ziweke vikwazo vya silaha kwa Sudan, kuwachukulia hatua wahusika wa uhalifu wa kivita na kutuma ujumbe wa kijeshi kuwalinda raia.
(Nairobi, Mei 9, 2024) – Mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya Rapid Support (RSF) na wapiganaji wenza katika El Geneina, mji mkuu wa eneo la magharibi mwa Sudan la Darfur, kuanzia Aprili hadi Novemba mwaka wa 2023 yalisababisha vifo vya angalau maelfu ya watu, huku mamia ya maelfu wakiachwa wakimbizi, Shirika la Human Rights Watch lilisema katika ripoti iliyotolewa leo. Uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu mkubwa wa kivita ulifanywa katika dhamira ya utokomezaji na ufurushaji wa kikabila wa watu wa jamii ya Massalit na jamii nyingine zisizokuwa za Kiarabu katika eneo la El Geneina.
Ripoti hiyo ya kurasa 218, The Massalit Will Not Come Home; Ethnic Cleansing and Crimes Against Humanity in El Geneina, West Darfur, Sudan “Massalit Hawatarudi Nyumbani: Ufurushaji wa Kijamii na Uhalifu dhidi ya Binadamu eneo la El Geneina, Darfur Magharibi, Nchini Sudan” inaeleza kuwa wapiganaji wa Rapid Support Forces, na wanamgambo wa Kiarabu wanaowaunga mkono, wakiwemo kundi lililojihami la Third-Front Tamazuj, walilenga eneo jirani la El Geneina lenye idadi kubwa ya watu wa Massalit, katika msururu wa mashambulizi kuanzia Aprili hadi Juni. Hujuma hiyo iliendelea tena mapema mwezi wa Novemba. Washambuliaji walifanya madhila mengine kama kuwatesa watu, kuwabaka na kupora mali. Zaidi ya wakimbizi nusu milioni kutoka Darfur Magharibi wamekimbilia nchini Chad tangu Aprili mwaka jana. Kufikia mwishoni mwa Oktoba mwaka wa 2023, asilimia 75 walikuwa kutoka El Geneina.
“Wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na serikali zinaanza kuona janga linalonukia El Fasher, ukatili wa kiwango kikubwa uliofanywa huko El Geneina unapaswa kuchukuliwa kama onyo la ukatili unaoweza kutokea ikiwa hatua za pamoja hazitachukuliwa,” alisema Tirana Hassan, Mkurugenzi Mkuu wa Human Rights Watch. “Serikali, Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa wanahitaji kuchukua hatua sasa kuwalinda raia. “
Kuwalenga watu wa jamii ya Massalit na jamii nyingine zisizokuwa za Kiarabu kwa kuwatendea hujuma kubwa kwa lengo la kuwaondoa kabisa katika eneo hilo ni sawa na ufurushaji wa kikabila. Muktadha wa jinsi mauaji haya yalifanywa kunaibua pia uwezekano kuwa RSF na washirika wao wana nia ya kuangamiza kwa sehemu au kwa ujumla watu wa Massalit huko Darfur Magharibi, jambo ambalo linaonyesha kuwa mauaji ya kimbari yamekuwepo au yanafanyika huko.
Kati ya Juni Mwaka 2023 na Aprili 2023, Shirika la Human Rights Watch liliwahoji zaidi ya watu 220 nchini Chad, Uganda, Kenya na Sudan Kusini na pia eneo lililoathiriwa nchini Sudan. Watafiti pia walitathmini na kuchambua zaidi ya picha na video 120 za matukio hayo, picha za setailiti, na stakabadhi zilizotolewa na mashirika ya haki za binadamu ili kuthibitisha taarifa za kutokea hujuma kubwa dhidi ya binadamu.
Vurugu zilizotokea El Geneina zilianza siku tisa baada ya vita kuanza Khartoum, mji mkuu wa Sudan, kati ya Jeshi la Sudan (SAF), na vikosi vya Rapid Support (RSF). Asubuhi ya Aprili tarehe 24, RSF walikabiliana na msafara wa Jeshi la Sudan uliokuwa ukipita katika eneo la El Geneina. Kisha RSF na washirika wao wakashambulia maeneo jirani yaliyokuwa na watu wa jamii ya Massalit, na kukabiliana na makundi yaliyojihami ya jamii hiyo waliokuwa wakitetea jamii zao. Katika majuma kadhaa yaliyofuatia, na hata baada ya makundi yaliyojihami ya Massalit kupoteza udhibiti wa eneo lao, RSF pamoja na wapiganaji wenza wenye silaha waliamua kulenga raia wasiokuwa na silaha.
Vurugu hizo zilifikia kilele chake pale kulitokea mauaji ya halaiki Juni tarehe 15, wakati RSF na washirika wao walishambulia msafara mrefu - kilomita kadhaa, wa raia waliokuwa wakijaribu kutoroka vita, wakisindikizwa na wapiganaji wa Massalit. RSF na wapiganaji wenza waliwafuata, wakawazunguka na kuanza kuwafyatulia risasi wanaume, wanawake na watoto waliokimbia kupita kwenye mitaa au walijaribu kuogelea kwenye maji ya mto Kajja yanayokwenda kwa kasi. Wengi walizama. Watu wazee na waliojeruhiwa hawakuachwa
Kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 17 alielezea jinsi watoto 12 na watu wazima watano kutoka familia kadhaa waliuawa. “Wapiganaji wawili wa RSF walinyakua watoto kutoka kwa wazazi wao, na wazazi walipoanza kupiga mayowe wakilia, wapiganaji wengine wawili wa RSF waliwauwa kwa kuwafyatulia risasi. Kisha wakawarundika watoto hao eneo moja na kuwafyatulia risasi. Wakarusha miili yao kwenye mto na mali zao zikafuatishwa majini humo.”
Siku hiyo na katika siku zilizofuatia, mashambulizi yaliendelezwa kwa makumi ya maelfu ya raia waliokuwa wakijaribu kutorokea Chad, eneo hilo likirundikwa miili ya watu. Video zilizochapishwa wakati huo zinaonesha umati wa raia wakikimbilia usalama wao katika barabara inayounganisha El Geneina na Chad.
Shirika la Human Rights Watch pia lina taarifa za kuuawa kwa wakazi wa Kiarabu na kuporwa kwa maeneo ya Waarabu na wapiganaji wa Massalit wakitumia silaha huku vikosi vya Jeshi la Sudan vikitumia vilipuzi katika maeneo yenye watu wengi katika hali ambazo zilisababisha uharibifu na mauti kwa raia.
Vikosi vya RSF na wapiganaji washirika waliendeleza hujuma zao tena mwezi Novemba, wakilenga watu wa jamii ya Massalit ambao walikuwa wamepata hifadhi katika eneo la El Geneina la Ardamata, wakiwazunguka wanaume na vijana wa kiume wa Massalit. Kulingana na Umoja wa Mataifa, angalau watu elfu moja waliuawa.
Wakati wa ukiukaji huu wa haki za binadamu, wanawake na wasichana walinajisiwa na kubakwa na kuhujumiwa kingono, wafungwa waliteswa na kuhujumiwa. Washambuliaji waliharibu miundomsingi muhimu kwa raia, wakilenga maeneo yenye makazi ya watu, na shule katika maeneo yaliyokaliwa na watu wa Massalit. Walipora mali nyingi na kuteketeza makazi ya watu baada ya kuua wakazi wake na kuwalazimisha wengine waondoke.
Matendo haya yalifanywa kama sehemu pana na yenye mfumo maalumu wa mashambulizi dhidi ya jamii ya Massalit na watu wengine wa jamii za watu wasiokuwa Waarabu na hivyo ni uhalifu dhidi ya binadamu kupitia mauaji, mateso, na kuhamishwa kwa watu kwa lazima, Shirika la Human Rights Watch lilisema.
Uwezekano kuwa mauaji ya halaiki yamefanywa au yanaendelea kufanywa katika eneo la Darfur unahitaji hatua ya haraka kutoka kwa serikali na taasisi zote za kimataifa ili kuwalinda raia. Lazima zihakikishe kuwa uchunguzi unafanywa kubaini ikiwa kulikuwepo au kuna nia ya uongozi wa RSF na washirika wake kutokomeza kabisa au kwa sehemu watu wa jamii ya Massalit na jamii nyingine zisizokuwa za Kiarabu magharibi mwa Darfur, yaani kufanya mauaji ya halaiki. Ikiwa ndivyo, basi wachukue hatua kusitisha unyama huu na kuhakikisha wahusika wa upangaji huu wanawajibishwa kisheria.
Jamii ya Kimataifa lazima iunge mkono uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, na mataifa wanachama wa mahakama hiyo lazima yahakikishe ina raslimali za kifedha za kutosha na zinazohitajika katika bajeti yake ili kutekeleza wajibu wake Darfur.
Human Rights Watch inawatuhumu Kamanda wa RSF, Mohammed “Hemedti” Hamdan Dagalo, kakaye Abdel Raheem Hamdan Dagalo, Kamanda wa RSF Darfur Magharibi Joma’a Barakallah kuwa watu wanaowajibika katika kutoa amri kwa wapiganaji waliofanya uhalifu huu. Shirika la Human Rights Watch pia lilitaja washirika wa RSF, akiwemo Kamanda wa kundi la Tamazuj na viongozi wawili wa Kijamii wa jamii ya Kiarabu kuwa wanaofaa kuwajibishwa kwa uhalifu uliofanywa na wapiganaji.
Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na Muungano wa Afrika lazima ziwatume kwa dharura kikosi cha kuwalinda raia walio katika hatari nchini Sudan. Baraza la Usalama linafaa kuweka vikwazo vya silaha kwa wale waliohusika katika uhalifu Magharibi mwa Darfur, iwe watu au mashirika ambayo yanakiuka marufuku ya silaha. Umoja huo Wafaa kupanua marufuku ya biashara ya silaha iliyowekwa dhidi ya Darfur na kuisambaza Sudan nzima.
“Kwa Dunia kukosa kuchukua hatua wakati wa hujuma na uhalifu wa kiwango hiki hakuna sababu tosha, “Hassan alisema. “Serikali lazima ihakikishe wote waliohusika wanawajibishwa, ikiwemo kwa kuwekewa vikwazo na kuimarisha ushirikiano na ICC.”