(Dar es Salaam) -- Watumishi wa ndani wa Kitanzania wanaofanya kazi Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wanakumbana na saa nyingi za kazi, kutokulipwa mishahara, na unyanyasaji wa kimwili na kijinsia, haya yamesemwa na ripoti ya Human Rights Watch iliyotolewa leo. Sheria kandamizi za udhamini wa viza katika nchi hizo na mapungufu katika sera za Tanzania zinawaacha wanawake kupambana na unyonyaji.
Ripoti ya kurasa 100, “Kufanya kazi mithili ya Roboti’: Unyanyasaji wa Watumishi wa ndani wa Kitanzania huko Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu,” imeweka kumbukumbu namna serikali za Tanzania, Oman na UAE zinavyoshindwa kulinda watumishi wa ndani wahamiaji kutoka Tanzania. Mfumo wa udhamini-wa viza wa kafala unaotumiwa na Oman na UAE unawafunga watumishi kwa waajiri wao, na ukosefu wa ulinzi wa sheria za kazi unawaacha wafanyakazi kupambana na aina nyingi za unyanyasaji. Mapungufu katika sheria na sera za Tanzania za uajiri na uhamiaji yanawaweka wanawake wa Kitanzania kuanzia mwanzo katika hatari ya kunyanyaswa na kushindwa kutoa msaada unaojitosheleza kwa wafanyakazi wanaonyonywa.
“Watumishi wa ndani wengi wa Kitanzania walioko Oman na UAE wanafanyishwa kazi kupita kiasi, wanalipwa pungufu, na wananyanyaswa nyuma ya pazi,” anasema Rothna Begum, mtafiti wa haki za wanawake Mashariki ya Kati na Human Rights Watch. “Wafanyakazi ambao walikimbia waajiri wanyanyasaji au mawakala walituambia polisi au maofisa wa balozi zao waliwalazimisha kurudi, au iliwabidi waacha mishahara yao na kupoteza miezi kadhaa kukusanya fedha kwa ajili ya tiketi kurudi nyumbani.”
Watumishi wengi wa ndani katika nchi za Ghuba ni kutoka Asia, wengi kutoka Indonesia, Ufilipino, India na Sri Lanka. Kutokana na nchi hizi kuendelea kuongeza ulinzi na mahitaji ya kima cha chini cha mshahara kulinda watumishi wao wa ndani-na katika kesi nyingine kuzuia kabisa ajira za Ghuba - waajiri wengi wanageukia Afrika Mashariki, ambapo ulinzi ni dhaifu. Waajiri wa Ghuba mara nyingi wanafanikiwa kuwalipa wafanyakazi kutoka Afrika Mashariki pungufu zaidi ya wale kutoka nchi nyingine.
Maelfu ya watumishi wa ndani wa Kitanzania wako Mashariki ya Kati. Wakati baadhi wakiwa katika mazingira ya kazi yenye staha, wengi wanakumbana na unyanyasaji. Human Rights Watch ilifanya mahojiano na watu 87, ikiwa ni pamoja na maafisa wa Tanzania, vyama vya wafanyakazi, mawakala wa uajiri, na watumishi wa ndani wanawake 50 wa Kitanzania ambao walifanya kazi Oman au UAE. Nusu ya watumishi wa ndani walitokea Tanzania bara, na nusu nyingine kutoka Zanzibar, sehemu ya nchi ambayo ni kisiwa chenye kujitegemea kwa kiasi fulani.
Takribani wote walisema waajiri wao walitaifisha hati zao za kusafiria. Wengi walifanya kazi kwa saa nyingi kupita kiasi, hadi saa 21 kwa siku bila mapumziko au siku ya mapumziko. Walisema walikuwa wakilipwa pungufu ya walichoahidiwa au kutokulipwa kabisa, walilazimishwa kula chakula kilichoharibika au mabaki, wakikaripiwa na kutukanwa kila siku, na kunyanyaswa kimwili na kijinsia. Baadhi ya kesi hizi ni sawa na kazi za shuruti au biashara haramu ya kusafirisha binadamu kufanya kazi za shuruti. Walikuwa na njia finyu za kujinasua kutoka katika mazingira ya kazi ya kinyanyasaji.
“Basma N.,” 21, kutoka Dar es Salaam, alisema mwajiri wake alimlazimisha kufanya kazi saa 21 kwa siku na kumnyanyasa kimwili. Kaka wa mwajiri wake alijaribu kumbaka mara mbili. Alikimbia na kukamatwa kwa kushindwa kumlipa mwajiri wake gharama za ajira, ilimbidi aache mishahara yake ya miezi mitatu. Ikamlazimu kukopa pesa ya kununua tiketi kurudi nyumbani, alirudi Tanzania akiwa na hali mbaya kifedha, kimwili na kihisia kuliko alivyoondoka.
Oman na UAE zinabagua watumishi wa ndani katika sheria zao za kazi. Kanuni za Oman za 2004 za watumishi wa ndani ni dhaifu, huku zikiwa hazitoi adhabu kwa mwajiri anaekiuka, na ni nchi ya mwisho katika ukanda wa Ghuba ambayo haina sheria ya haki za kazi. Septemba 2017, UAE ilitangaza kwa mara ya kwanza sheria inayotoa haki za kazi kwa watumish wa ndani, lakini ulinzi ni dhaifu kuliko wafanyakazi wengine katika sheria ya kazi.
Mfumo wa kafala unaendelea kuwa kizuizi kikubwa kwa watumishi wa ndani huko Oman na UAE, na unapaswa kukomeshwa, walisema Human Rights Watch. Watumishi wa ndani hawawezi kubadili mwajiri bila ya ridhaa ya mwajiri wa awali, na wale wanaokimbia wanaweza kuadhibiwa kwa “kukimbia kazi.”
Baadhi ya wafanyakazi walisema kwamba waajiri au mawakala wao waliwalazimisha kuacha mishahara yao kama masharti ya “kuachiwa,” kufanya kazi na mwajiri mpya ambaye analipa gharama za uajiri kwa mwajiri wa awali, au kufanya kazi bila malipo kwa miezi kadhaa ili kupata tiketi ya kurudi nyumbani au kurejesha ada za uajiri. Huko Oman, polisi na maafisa wa Wizara ya Kazi wakati mwingine wanasaidia juhudi za waajiri kurudisha gharama zao kutoka kwa watumishi waliokimbia manyanyaso. Sheria mpya ya UAE inakataza mawakala kutoza ada au kuhitaji kurejeshewa ada za uajiri, lakini haizuii waajiri kufanya hivyo. Badala yake, inawataka watumishi wanaotaka kuondoka kabla ya mkataba kuisha, isipokuwa pale mwajiri anapovunja mkataba, kumlipa mwajiri mshara wa mwezi mmoja.
Wakati Tanzania imepanua baadhi ya ulinzi kwa watumishi wa ndani wahamiaji tangu 2011, mapungufu katika sera za Tanzania za ajira na uhamiaji yanawaweka wafanyakazi katika hatari kuanzia mwanzo na kutoa njia finyu za kufidiwa.
Tanzania inawataka wafanyakazi wapitishe maombi ya kuhama kupitia wizara za kazi nchini, lakini wafanyakazi wengi wanahama nje wa mfumo huu.
Mamlaka zinawataka wanawake kuhama kupitia wakala wa uajiri lakini hazijaweka viwango vya chini vya namna mawakala wanapaswa kuwasaidia watumishi wanapokutana na unyanyasaji, au ukaguzi na adhabu pale wanapokiuka. Wakati kanuni za Tanzania bara na Zanzibar zinakataza mawakala kutoza ada na gharama kwa watumishi, wanawake wengi wanasema pamoja na hayo mawakala bado wanawatoza.
Viwango vya mkataba vya Tanzania kwa watumishi wa ndani walioko Oman na UAE vinatoa kiwango cha chini cha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi. Hata hivyo, watumishi wengi wa ndani wanasema waajiri wao hawaheshimu mkataba. Kwa kiasi fulani hii inatokana na mikataba ya Tanzania kukosa msukumo wa kisheria huko Oman na UAE. Balozi za Tanzania zinakosa mfumo unaojitosheleza wa ulinzi, na hazina nguvu ya kumsaidia mtumishi kumlazimisha mwajiri kurejesha mishara ambayo haijalipwa, kulipa fidia, au kulipia tiketi ya ndege kurudi nyumbani.
Tanzania pia haina utaratibu wa kushughulikia malalamiko au mfumo wa kutoa msaada wa matibabu kwa watumishi wanaorejea ambao wamepitia unyanyasaji au unyonyaji ughaibuni. Ukosefu wa sera za kuwezeshwa kiuchumi zinawaacha wanawake wengi kutaka kuhama kwa mara nyingine hata pale wanapokuwa wamekumbana na manyanyaso.
Tanzania haina budi kupitisha mikakati maalumu kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja kanuni kali na uangalizi wa uajiri, programu za mafunzo ya haki, na msaada wa kujitosheleza kutoka katika balozi ikiwa ni pamoja na kulipa gharama za tiketi kurudi nyumbani, walisema Human Rights Watch.
“Tanzania inapaswa kuhakikisha kwamba wanawake wanaweza kuhama kwa usalama kwa ajili ya kazi za ndani,” alisema Begum. “Tanzania, Oman an UAE lazima zifanye kazi kwa pamoja kuzuia unyonyaji wa watumishi wa ndani wahamiaji, kuchunguza unyanyasaji, na kuwashitaki wale wanaohusika.”
“Atiya Z.,” 28, kutoka Kondoa, alisafiri kwenda Oman mwezi Juni 2015. Anasema mwajiri wake alitaifisha hati yake ya kusafiria na simu yake, alimlazimisha kufanya kazi saa 21 kwa siku bila mapumziko au siku ya mapumziko, hakumruhusu kula bila ruhusa yake, na alikuwa akimpiga kila siku. Alijaribu kukimbia baada ya wiki tatu, lakini mwajiri wake alimrudisha na kumtaka amlipe gharama za ajira kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 2(US$880). Baada ya hapo, anasema, mwajiri wake alimfungia ndani ya nyumba. Mwezi Aprili 2016, anasema alizimia kutokana na kushindwa kula kwa sababu ya kuvimba koo. Aliporudi kutoka hospitali, mwajiri wake alilipiza kisasi: “Yule mwanamke alianza kunipiga na kusema: ‘Hukuja hapa kuumwa.’ Alimuita wifi yake, ambae alikuja kisha wakanivua nguo na kunipiga na vitundikio vya nguo. Mafundi ujenzi walikuwa wakiniskia nikipiga kelele kutokea nje lakini hawakuweza kunisaidia. Mumewe aliporudi alinipeleka chumbani kisha kunibaka kwa kuniingilia kinyume cha maumbile. Baada ya kumaliza kunibaka, walinipeleka kwenye nyumba ya kaka yao na siku iliyofuata walinipandisha kwenye ndege kurudi Tanzania. Walichukua pesa zangu nilizoingiza, na kunirudishia hati yangu ya kusafiria. Waliniacha uwanja wa ndege. Nilikuwa naogopa, mwenye maumivu, na sikujua nani wa kuongea nae.”
“Inaya R.,” 23, anasema mwaka 2013 mwajiri wake huko Oman hakumlipa kwa miezi mitano lakini alipotaka kuondoka, walimdai gharama za uajiri kiasi cha 700 OMR (US$1,818). Ubalozi haukuweza kupata mwajiri mpya ambaye alikuwa tayari kulipa kiasi hicho, hivyo alirudi nyumbani bila mshahara na ilimbidi kutafuta pesa zake mwenyewe kulipia gharama zake za tiketi kurudi nyumbani. “Ubalozi hauna nguvu ya kusema chochote,” anasema.
“Hidaya Z.,” 30, anasema kwa takribani miaka miwili, mwajiri wake alimlazimisha kufanya kazi kwa saa 17 kwa siku bila mapumziko, wala siku ya mapumziko, akimfungia ndani ya nyumba pale wanapotoka nyumbani, akimtukana, akimlipa 50 OMR ($130) badala ya 80 OMR ($208) ambayo mkataba wake umeelekeza, na kushindwa kumlipa mishahara ya miezi sita. Mwishowe mwaka 2016 alikimbia baada ya mwanafamilia mmoja wa kiume kumshambulia kingono. Alienda kufungua malalamiko polisi ili kupata hati yake ya kusafiria kutoka kwa mwajiri wake baada ya kushauriwa na ubalozi wa Tanzania Oman. Polisi walimwambia mwajiri wake alikuwa amefungua mashitaka dhidi yake kwa kukimbia.
Anasema: “Niliwaeleza polisi matatizo yangu lakini hawakujali.” Polisi walimuambia alipe 200 OMR ($520) au kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela. Anasema alirudi ubalozini, ambapo alitumia miezi mitatu kukusanya fedha za kulipia faini. “Vitu vyangu vyote, ikiwa ni pamoja na nguo mpya nilizonunua kwa ajili ya familia yangu na simu yangu, niliacha kwenye nyumba [ ya mwajiri] [nilipokimbia] na kurudi kama unavyoniona.” Anasema.