(Kampala) – Serikali ya Tanzania inapaswa kuwaruhusu wafungwa wote kupata ushauri wa kisheria ili kuhakikisha haki zao zinaheshimiwa kipindi hiki cha janga la Covid-19, Human Rights Watch wamesema hii leo. Mnamo Mei 9, 2020, mashirika 20 ya haki za binadamu ikiwa ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Dar es Salaam, Amnesty International na Human Rights Watch walituma barua kwa Rais wa Tanzania John Magufuli, kutaka mamlaka kuhakikisha kuwa wafungwa wote na walio vizuizini na mahabusu wanaweza kupata wanasheria na kuchukua hatua kupunguza msongamano katika magereza.
Mnamo Machi 19, mamlaka ya magereza ilizuia wafungwa kutembelewa katika magereza zote nchini kwa kipindi kisichojulikana ili kuepuka maambukizi ya Covid-19. Marufuku hii iliwajumuisha wanasheria, kitu ambacho kimemnyima mfungwa nafasi ya kupata ushauri wa kisheria na kupunguza kasi ya kukiri makosa, kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali na kutatuliwa kwa kesi, wanasheria waliwaambia Human Rights Watch.
“Zuio la wageni kutembelea magereza limemaanisha kuwa walio kizuizini hawawezi kuzungumza na wanasheria wao, kitu ambacho kinawanyima haki ya kupata hukumu yenye usawa,” alisema Oryem Nyeko, mtafiti wa Afrika kutoka Human Rights Watch. “Serikali imechukua hatua muhimu kupunguza kusambaa kwa maambukizi ya Covid-19, lakini hili halipaswi kufanywa kwa gharama ya haki za msingi.”
Hadi sasa Tanzania imeripoti kesi 509 za maambukizi ya Covid-19, na serikali imetilia mkazo suala la watu kukaa umbali wa mita moja na uvaaji wa barakoa. Hata hivyo, hakuna katazo la watu kutembea na shughuli za mahakama zinaendelea. Washtakiwa hawaruhusiwi kufika mahakamani kusikiliza kesi isipokuwa kupitia video kwa magereza ambazo vifaa hivi vinapatikana.
Wanasheria waliwaambia Human Rights Watch kuwa zuio la kutembelea magereza linamaanisha kwamba hawatoweza kuzungumza na wateja wao na kushindwa kuwawakilisha ipasavyo, kutokana na kwamba hawawezi kuonana nao ana kwa ana na hakuna utaratibu wowote wa kuzungumza nao kwa faragha kupitia simu. Wanasheria wawili walisema mahakama imewapangia wateja wawili ambao hawajawahi kuongea nao kutokana na zuio hili. Mamlaka za Tanzania hazijafanya juhudi zozote kuweka njia mbadala kwa wanasheria kuwafikia wateja wao walioko kizuizini kupitia simu zenye usalama au mikutano kwa njia ya video.
Utaratibu wa kukiri makosa, kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali, ambao serikali iliuweka mwaka 2019 kwa lengo la kupunguza msongamano katika magereza na katika mahakama hauwezi kufanya kazi ikiwa washtakiwa hawawezi kukutana na wanasheria wao kujadili kesi zao. Wanafamilia hawawezi kuonana na wapendwa wao walioko kizuizini na hawawezi kuwapelekea chakula, kitu kinachowalazimisha kula chakula cha magereza ambacho kwa mujibu wa mwanasheria mmoja ni chakula kisicho na ubora.
Magereza za Tanzania zina msongamano jambo ambalo linaweza kusababisha hatari za kiafya kwa wafungwa. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, magereza nchini zimezidiwa uwezo kwa asilimia 9 na haziruhusu suala la watu kukaa umbali wa mita moja, jambo ambalo linaleta mazingira ya uwezekano wa virusi kusambaa zaidi.
Mnamo Aprili 25, Rais Magufuli alisamehe wafungwa 3,717, sambamba na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kupunguza msongamano katika magereza ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa. Hata hivyo, magereza nchini zimeendelea kuwa na msongamano.
Serikali ya Tanzania inapaswa kuchukua hatua za haraka kupunguza idadi ya wafungwa, ikiwa ni pamoja na kupitia kesi za mahabusu, ambao ni sehemu kubwa ya wafungwa walioko gerezani. Pia inapaswa kutekeleza njia mbadala kwa wanasheria kuwasiliana na wateja wao, kupitia simu zenye usalama au mfumo wa video.
Serikali ina jukumu la kuhakikisha haki ya afya kwa wafungwa, walioko kizuizini na watu wengine walionyimwa uhuru. Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu, ambalo linazingatiwa kuakisi sheria za kimataifa, linamhakikishia kila mmoja haki ya kupata hukumu yenye usawa na kuwakilishwa na mwanasheria. Kiwango cha Chini cha Sheria za Umoja wa Mataifa juu ya Kuhudumia Wafungwa (Sheria za Nelson Mandela) pia zinaeleza haki ya kuwakilishwa kisheria. Katiba ya Tanzania inampa kila mmoja haki ya “kusikilizwa kwa usawa” mbele ya mahakama.
“Msongamano katika magereza nchini Tanzania unaongeza hatari kubwa kwa afya ya wafungwa hususan katika kipindi hiki cha janga la Covid-19,” anasema Nyeko. “Serikali inapaswa kuweka kipaumbele suala la kupunguza msongamano zaidi na kuboresha hali za magereza ili kila mfungwa awe salama.”